Upinzani hauna mpango, asema Rais Ruto wakati akitoa wito wa amani

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto ameukosoa upande wa upinzani nchini akisema hauna mpango wala ajenda yoyote ya kuwanufaisha Wakenya. 

Akilaani siasa za ukabila, ametoa wito kwa Wakenya kuungana katika kuitumikia nchi kwa umoja na kuepukana na migawanyiko miongoni mwao.

Kiongozi wa nchi aidha amelaani machafuko ambayo yamekuwa yakishuhudiwa nchini akisema hayawezi kamwe kuleta maendeleo.

“Vijana hawawezi wakapata ajira ikiwa kuna vurugu na machafuko. Tunataka kuwepo kwa amani ili tuweze kutekeleza mipango yetu,” aliongeza Rais Ruto wakati akihutubia mamia ya wakazi katika eneo la Embakasi, kaunti ya Nairobi.

Rais Ruto amekuwa mstari wa mbele katika kuukemea upande wa upinzani akiushutumu kwa kucheza siasa zilizojikita kwa misingi ya ukabila na migawanyiko.

Si hayo, alikuwa na ujumbe kwa wakazi wa jiji la Nairobi.

Ruto akisema utawala wake umezindua mpango ambao utabadilisha sura ya jiji la Nairobi ili kulifanya kuwa kituo kinara cha biashara duniani.

Katika awamu ya kwanza, Rais alisema serikali itajenga kilomita zisizopungua 70 za barabara jijini Nairobi ili kuwezesha biashara, kupunguza msongamano wa magari na kuchochea ukuaji.

 

Share This Article