Muungano wa wanamuziki wa Uganda UMA na shirikisho la kitaifa la wanamuziki nchini Uganda UNMF zimeafikia makubaliano na kuahidi kushirikiana kwa manufaa ya wanachama wao.
Mwanamuziki Cindy Sanyu ambaye ni rais wa UMA alifichua kwamba makubaliano hayo yaliafikiwa wiki kadhaa zilizopita, na mkataba wa maelewano ulitiwa saini.
Kulingana naye, vyama hivyo viwili vya kutetea maslahi ya wanamuziki vilikubaliana kushirikiana ili kuafikia lengo moja, lakini sio katika kila nyanja.
Sanyu alikubali kwamba awali kulikuwa na kutoelewana kati ya makundi hayo mawili akiongeza kusema kwamba yapata wiki mbili zilizopita waliketi kama viongozi wakakubaliana kushirikiana.
“Tuliketi chini nao na tukaamua kutia saini mkataba wa maelewano, kuhusu namna ya kushirikiana na sasa tunashirikiana,” alisema mwanamuziki huyo.
Makundi hayo mawili yanaazimia kulainisha juhudi zao kwa masuala makuu yanayoathiri wanamuziki wa Uganda kama vile kulinda hakimiliki, maslahi ya wasanii na maendeleo ya kitaaluma.
Muungano wa wanamuziki wa Uganda UMA ambao kwa sasa unaongozwa na Cindy Sanyu ambaye ni rais ulianzishwa Novemba 28, mwaka 2017 kwa lengo la kulinda, kutangaza na kuhifadhi muziki wa Uganda na kupigania maslahi ya wanachama.
Shirikisho la kitaifa la wanamuziki nchini Uganda UNMF ambalo linaongozwa na Eddy Kenzo kama rais na Sheebah Karungi na Palasso kama wasaidizi wake, liliasisiwa mwaka 2023, ili kuwa jukwaa la sauti moja ya tasnia ya muziki nchini Uganda.