Tarehe 8 mwezi Machi kila mwaka, ni siku iliyotengwa na Umoja wa Mataifa kusherehekea siku ya kimataifa ya wanawake.
Siku hii huadhimishwa kutafakari hatua zilizopigwa na wanawake, vikwazo kwa maendeleo yao katika jamii, na kutafakari kuhusu suluhisho mwafaka.
Kufikia sasa, mataifa 193 kote ulimwenguni yamebuni sera 1,583, za kuwainua wanawake na nyingine 354 za kukabiliana na dhuluma za kijinsia.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaandaliwa chini ya kaulimbiu “kwa wanawake wote na wasichana, haki, usawa na uwezeshaji.”
Sherehe za mwaka huu pia zitafungamana na maadhimisho ya miaka 30, tangu kuandaliwa kwa kongamano la kimataifa la wanawake maarufu kama Beijing Conference.
Hapa nchini, serikali imebuni sera za kuwapiga jeki wanawake kama vile mikopo ya kibiashara, kutunga sera za kukabiliana na dhuluma dhidi ya wanawake kama vile ukeketaji, ndoa za watoto, dhuluma za kijinsia, na ubaguzi.
Maadhimisho hayo yanaandaliwa wakati pia jopokazi kuhusu jinsia lililoteuliwa na Rais likiandaa ripoti ya kutafuta suluhu kwa dhuluma dhidi ya wanawake kama vile dhuluma za kijinsia na mauaji ya wanawake kikatili na wapenzi wao.