Ulaghai hautashuhudiwa SHA, aahidi Rais Ruto

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais William Ruto akiwa na viongozi wengine wakati wa mazishi ya mbunge Malulu Injendi

Rais William Ruto amewahakikishia Wakenya kuwa hakuna punje ya ufisadi itakayoshuhudiwa katika Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). 

Rais Ruto anasema wale wanaopinga mfumo mpya wa SHA ni matapeli ambao walifaidi kutokana na Hazina ya Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) iliyovunjwa.

Akizungumza katika eneo bunge la Malava wakati wa mazishi ya aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Malulu Injendi, Rais Ruto alisifia bima mpya ya afya akisema ilisaidia kugharimia matibabu ya marehemu mbunge huyo yenye kima cha shilingi milioni 9 alipokuwa amelazwa katika hospitali moja jijini Nairobi.

“Hii makelele ya mtandao ni watu walikuwa wanatuibia siku za NHIF. Hakuna senti ya serikali itatumiwa kulipa system yoyote,” alisema kiongozi wa nchi.

Kiongozi wa nchi akitumia fursa hiyo kuwasihi wakazi kujiandikisha kwa SHA ili kunufaika na huduma bora za matibabu.

Matamshi yake yanakuja ambapo Mkaguzi Mkuu Nancy Gathungu ametilia shaka usimamizi wa SHA katika hatua ambayo imeibua mashaka juu ya fedha zinazochangwa na Wakenya kwa mfumo huo.

Kwa muda sasa, Wakenya wamekuwa wakilalamikia huduma mbovu zinazotolewa chini ya SHA wakisema wanalazimika kugharimia matibabu yao wenyewe.

Rais Ruto amekiri kuwa ingawa kuna changamoto katika uendeshaji wa mfumo huo, hatimaye utafanya kazi kama ilivyokusudiwa.

Share This Article