Wazazi na wanafunzi wa zamani wamelalamikia kile wanachokitaja kuwa ukosefu wa miradi ya hazina ya kitaifa ya maendeleo ya maeneo bunge NG-CDF, katika shule kama ile ya msingi ya Kihumbu Ini.
Shule hiyo ambayo iko kwenye eneo bunge la Kinangop katika kaunti ya Nyandarua, inaripotiwa kuwa na wanafunzi wengi kutoka eneo bunge la Kipipiri.
Hali hiyo imesababisha viongozi wa maeneo bunge hayo mawili kukosa kushirikiana na hivyo jamii ya eneo hilo imeachwa bila usaidizi unaofaa.
Shule ya msingi ya Kihumbu Ini ni muhimu kwani huwa inatumika kama kituo cha kupigia kura, lakini inakumbwa na changamoto katika kupokea raslimali hitajika na miradi ya maendeleo.
Wazazi, wanafunzi wa zamani na usimamizi wa shule sasa wanatoa wito kwa wabunge Kwenya Thuku wa Kinangop na Wanjiku Muhia wa Kipipiri waungane kwa ajili ya manufaa ya watu wa eneo hilo badala ya kugawanyika kwa sababu ya mipaka ya maeneo bunge.
Mwenyekiti wa muungano wa wanafunzi wa zamani wa shule ya msingi ya Kihumbu Ini, Munene Njuguna, naye ameomba wanafunzi wote wa zamani warejee na watoe mchango ili kumotisha wanafunzi wa sasa.
Kulingana naye mpango huo unaweza kumotisha wanafunzi na kuwajibisha wanajamii.
Wito wa ushirikiano na umoja katika mpaka wa maeneo bunge hayo mawili unaweza kuwa muhimu katika kuchochea maendeleo na kuwezesha wakazi.