Ujenzi wa barabara ya kilomita 170 ya Rironi-Mau Summit, inatarajiwa kuanza katika muda wa miezi mitatu ijayo.
Kulingana na wizara ya Barabara na Uchukuzi, mwanakandarasi atakayejenga barabara hiyo anatarajiwa kufika eneo la ujenzi ili kushughulikia swala la msongamano wa magari utakaosababishwa na ujenzi huo.
Hatua hii inajiri baada ya serikali kutangaza kuwa Iko katika harakati za kufuatilia mbali kandarasi ya awali, iliyokuwa imekabidhiwa kundi la makampuni ya ufaransa na serikali iliyopita.
Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir, alisema ujenzi wa barabara hiyo ya moja kwa moja ni lazima utekelezwe kutokana na idadi ya shughuli za uchukuzi zinazoongezeka kila uchao kati ya Rironi na Mau Summit.
“Mwanakandarasi atakuwa katika eneo la ujenzi katika muda wa miezi miwili au mitatu na kuhusu iwapo barabara hiyo itafungwa au la, swala hilo tutaliangazia karibuni,” alisema ChirChir.
Waziri huyo aliyasema hayo alipokuwa akiwahutubia wanahabari katika hoteli moja mjini Naivasha, baada ya kukutana na kamati ya bunge la Senate kuhusu Barabara na Uchukuzi.
Kuhusu ongezeko la ajali za barabarani hapa nchini, Waziri huyo alisema serikali imechukua hatua kabambe ikiwa ni pamoja na kuweka kamera za barabarani, kuimarisha misako barabarani pamoja na kubuni mfumo wa usimamizi wa trafiki.