Ugonjwa usiojulikana wasababisha hofu Mombasa

Tom Mathinji
1 Min Read
Ugonjwa usiojulikana wasababisha hofu Mombasa.

Wakazi wa Migadini, Changamwe, kaunti ya Mombasa, wanaishi kwa hofu baada ya ugonjwa usiojulikana kusababisha vifo vya watu wanne katika hali isiyoeleweka.

Kulingana na wakazi hao,miili ya waathiriwa hufura na ngozi yao hubambuka, tukio ambalo limezua hofu kubwa.

Aidha, maafisa wa afya wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha vifo hivyo, huku sampuli zikipelekwa katika Taasisi  ya Utafiti wa Kimatibabu (KEMRI) kwa uchunguzi.

“Idara ya Afya ya kaunti ya Mombasa imepokea habari ambazo hazijathibitishwa kuhusu vifo vya watu wanne kwa njia tatanishi. Idara hiyo imetuma wachunguzi katika eneo la Migadini, kuchunguza ripoti hiyo,” ilisema idara ya afya kaunti ya Mombasa.

Maafisa wametoa wito kwa wakazi hao wawe watulivu na kuzingatia usafi huku uchunguzi ukiendelea.

“Serikali ya kaunti inaendelea kukadiria hali na itatoa habari zaidi punde tu itakapozipokea,”iliongeza taarifa hiyo.

Hata hivyo, maafisa wa utabibu wamesema waathiriwa hao walikuwa wanaugua hapo awali.

TAGGED:
Share This Article