Uganda yathibitisha kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola

Tom Mathinji
2 Min Read
Uganda yatangaza kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola.

Uganda imethibitisha kuzuka kwa ugonjwa wa virusi vya Ebola katika mji mkuu Kampala.

Kulingana na wizara ya afya nchini humo, mgonjwa wa kwanza ambaye ni muuguzi  mwenye umri wa miaka 32, alifariki kutokana na makali ya ugonjwa huo siku ya Jumatano.

Wizara hiyo ilisema kuwa mgonjwa huyo awali alikuwa ametafuta matibabu katika vituo mbalimbali vya afya, ikiwemo hospitali ya Mulago baada ya kupata dalili za homa, maumivu ya kifua na kupata shida kupumua.

“Mgonjwa huyo ni mwanamume mwenye umri wa miaka 32, ambaye ni muuguzi katika hospitali ya kitaifa ya rufaa ya Mulago, ambaye alitafuta matibabu katika vituo mbali mbali vya afya,” ilisema taarifa ya wizara ya afya ya Uganda.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, mgonjwa huyo kwanza alionyesha dalili za homa kali, maumivu ya kifua na ugumu wa kupumua. Baadaye alivuja damu kutoka kwa viungo vingi vya mwili kabla ya na kusababisha kifo chake.

“Mgonjwa huyo alikuwa na historia ya kuugua homa kali iliyodumu siku tano na ugumu wa kupumua kabla ya kuanza kujuva damu kutoka sehemu kadhaa za mwili,” iliongeza taarifa hiyo.

Wizara hiyo imesema imechukua hatua kadhaa kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutuma kundi la maafisa wa afya kuwatambua wale wote waliotangamana na mgonjwa huyo, huku ikisema kuwa takriban watu 45 waliotangamana na mgonjwa huyo tayari wametambuliwa. Wao ni pamoja na wahudumu na wagonjwa 30 katika hospitali ya Mulago, watu 11 ambao ni wa familia ya mwathiriwa huyo na wahudumu 4 wa hospitali ya Saidina Abubakar ambako mgonjwa huyo alikwenda kwa matibabu.

Uganda ilikumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo mwishoni mwa mwaka wa 2022, kabla ya  kutangazwa kuwa ulikuwa umedhibitiwa Januari mwaka wa 2023.

Mlipuko wa mwisho wa ugonjwa huo uliwaua watu 55 kati ya 143 walioambukizwa wakiwemo wafanyikazi sita wa afya.

TAGGED:
Share This Article