Uganda yakomesha matumizi ya sarafu za kigeni katika manunuzi

Lengo kuu ni kupunguza hatari ya ongezeko la gharama linalosababishwa na mabadiliko ya ghafla ya viwango vya ubadilishaji wa sarafu za kigeni duniani.

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali ya Uganda imetoa agizo kali linalopiga marufuku mikataba yote ya sekta ya umma na michakato ya ununuzi kufanywa kwa kutumia sarafu za kigeni na kuimarisha matumizi ya Shilingi ya Uganda katika miamala yote.

Ramadhan Ggoobi, ambaye ni katibu wa kudumu na Katibu wa Hazina, alitangaza hatua hiyo katika Waraka wa Utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.

Alisema hatua hiyo ni muhimu kulinda uthabiti na ushindani wa sarafu ya ndani.

Agizo hilo linaendana na sheria ya usimamizi wa fedha za umma ya Uganda na linajiri baada ya Rais Yoweri Museveni kuidhinisha mswada wa ugawaji fedha kwa mwaka wa fedha 2025/26 mnamo tarehe 30 Juni 2025.

Mwongozo huo mpya unataka mikataba yote ya serikali, isipokuwa ile inayofadhiliwa moja kwa moja kwa mikataba ya fedha kutoka nje, itanukuliwe na kulipwa kwa kutumia Shilingi ya Uganda.

Maafisa wa Uhasibu katika taasisi zote za serikali sasa wametakiwa kuzingatia kwa ukamilifu mwongozo huu.

Hii inamaanisha kuwa ununuzi wote uliopangwa, iwe kupitia mfumo wa ununuzi wa kielektroniki au mfumo jumuishi wa usimamizi wa fedha, lazima ufanyike kwa kutumia Shilingi ya Uganda.

Ggoobi alisema lengo kuu ni kupunguza hatari ya ongezeko la gharama linalosababishwa na mabadiliko ya ghafla ya viwango vya ubadilishaji wa sarafu za kigeni duniani.

Zaidi ya hayo, mikataba yote, hata ile inayofanywa kwa ushindani wa kimataifa, itanukuliwa kwa Shilingi ya Uganda, isipokuwa tu mikataba ya fedha ambapo Washirika wa Maendeleo wanahitaji wazi matumizi ya sarafu za kigeni katika mchakato wa zabuni na malipo.

Share This Article