Uganda kuhamisha raia wake walio Iran

Iran na Israel zinazozozana, zimefunga anga zao na hivyo kufanya usafiri wa wanaotoroka nchi hizo kuwa mgumu.

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali ya Uganda imeanzisha mipango ya kuhamisha raia wake walioko Iran kufuatia mapigano kati ya Iran na Israel yaliyoanza Juni 13, 2025.

Wizara ya masuala ya kigeni ya taifa hilo la Afrika Mashariki imethibitisha kwamba raia wake 42 tayari wameondolewa Tehran, mji mkuu wa Iran inaposhirikisha balozi zake na mashirika husika ya serikali kuhakikisha uhamisho salama wa waganda waliosajiliwa nchini humo.

Inahusisha hata nchi jirani kufanikisha uhamisho salama wa watu hao mchakato ambao umekumbwa na changamoto kufuatia hatua ya Iran ya kufunga anga yake na hivyo kufanya usafiri kuwa mgumu.

Iran na Israel zimefunga anga zao kwa muda usiojulikana na Uganda imewasiliana na serikali za nchi kama Uturuki, Azerbaijan, na Jordan, kuona iwapo zitaruhusu raia wake waingie humo bila visa kuhakikisha usalama wao.

Balozi za Uganda nchini Uturuki, Saudi Arabia, Milki za Kiarabu na Qatar zimeagizwa kutoa usaidizi wa kibalozi kwa raua wa Uganda wanaopitia nchi hizo kutoka Israel na Iran.

Mapigano kati ya Israel na Iran yako katika wiki ya pili sasa, huku Israel ikilenga kituo cha utafiti wa silaha za nyuklia cha Iran huku Iran ikionya Marekani dhidi ya kuingilia vita hivyo.

Huku hayo yakijiri, Rais wa Marekani Donald Trump, ametangaza kwamba wameshambulia vituo kadhaa vya nyuklia vya Iran.

Share This Article