Wabunge wanaogemea mrengo wa Kenya Moja sasa wanamtaka Waziri wa Afya Aden Duale kujiuzulu.
Wakiwahutubia wanahabari na kuongozwa na Seneta wa Nairobi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna, wabunge hao wamemtaka Duale kujiuzulu katika kipindi cha saa 48 zijazo la sivyo wawasilishe hoja ya kumbandua kwenye wadhifa huo punde bunge litakaporejelea vikao vyake mwishoni mwa mwezi ujao.
Kiini cha wao kumtaka Duale kuachia ngazi ni madai kwamba Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA inateuka uvundo wa ufisadi.
Wabunge hao wanamtuhumu Duale kwa kushindwa kukomesha ufisadi kwenye mamlaka hiyo ambao umesababisha walipa kodi kupoteza mabilioni ya pesa.
Aidha, wameongeza kuwa wamepata ushahidi wa kuonyesha kuwa kuna mgongano wa maslahi katika uendeshaji wa SHA.
Wametaja ubaguzi katika utoaji wa malipo ya hospitali zinazotoa huduma kwa wagonjwa chini ya SHA, huk baadhi ya hospital zikipendelewa wakati zingine zikikosa kuambulia chochote.
Sasa wamempa mwenyekiti na mkurugenzi mtendaji wa SHA makataa sawia wakitoa wito kwa mamlaka hiyo kufanyiwa mageuzi ya jumla ili kuboresha utenda kazi wake.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, mbunge wa Kitutu Chache Anthony Kibagendi alisema wakati Hazina ya Bima ya Kitaifa, NHIF ilipofungwa, ilikuwa na deni la jumla ya shilingi bilioni 32.
Lakini chini tu ya miezi 10 tangu kuzinduliwa kwake, mbunge huyo alidai SHA inadaiwa shilingi bilioni 43.
Madai yao yanakuja wakati ambapo Waziri Duale ameapa kukabiliana na visa vya udanganyifu kutokana na madai ya malipo ya kutilia shaka yanayowasilishwa na hospitali malimbali nchini.
Tayari SHA imekataa kulipa kitita cha shilingi bilioni 10 kwa baadhi ya hospitali kutokana na madai ya ulaghai.