Jumla ya wawaniaji saba wa chama cha UDA wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kukabidhiwa vyeti vya muda kugombea nyadhifa za uwakilishi wadi na ubunge kwenye uchaguzi mdogo ujao ulioratibiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Wawaniaji hao sasa hawatashiriki uchaguzi wa mchujo wa chama hicho uliopangwa kufanyika Septemba 20.
Wawaniaji 3 wanamezea mate nyadhifa za ubunge katika maeneo ya Mbeere Kaskazini, Magarini na Banisa huku wawaniaji wanne wakipania kuwa wawakilishi wadi katika maeneo ya Fafi, Purko, Chewani na Angata Nanyukie.
Mwenyekiti wa chama tawala cha UDA Cecily Mbarire ambaye pia ni Gavana wa Embu amehawakikishia wawaniaji wa tiketi ya chama hicho uchaguzi huru wa mchujo.
Amesema kama UDA, watasimamisha wagombea wengi kwenye uchaguzi huo huku katika baadhi ya maeneo, chama hicho kikisikizana na vyama vingine kuwasilisha mgombea mmoja.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC imetangaza kuwa chaguzi ndogo 24 zitaandaliwa katika maeneo mbalimbali nchini Novemba 27.