Uchaguzi wa kamati ya kitaifa ya Olimpiki nchini – NOCK, uliokuwa umesubiriwa kwa hamu na ghamu, leo umeahirishwa kwa majuma mawili, baada ya mashirikisho manne kushindwa kuelewana kuhusu wajumbe wanaopaswa kupiga kura.
Licha ya Rais wa kamati ya NOCK, Paul Tergat, kujaribu kusuluhisha swintofahamu hiyo, mashirikisho ya mpira wa mikono, voliboli, triathlon na taekwondo yalikosa kuafikiana kuhusu ni nani anayepaswa kupiga kura baina ya Wenyeviti na Makatibu, na kulazimisha kuahirishwa kwa uchaguzi ambao ulikuwa ajenda ya mwisho katika mkutano mkuu wa mwisho wa mwaka.
Mashirikisho 25 yalikuwa yameidhinishwa kushiriki uchaguzi huo ambao umenashuhudia upande mbili moja ikiongozwa na Naibu Rais wa kwanza Shadrack Maluki na Katibu Mkuu Francis Mutuku, wanaotaka kumrithi Tergat, ambaye amekamilisha muhula wake wa miaka minane afisini.
Uchaguzi huo awali ulikuwa umecheleweshwa kwa muda kusubiri uamuzi wa kesi zilizowasilishwa mahakamani.
Kamati kuu ya NOC, itakutana na kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi huo unaotarajiwa katika kipindi cha majuma mawili yajayo.
Nyadhfa 12 zinawaniwa kwenye uchaguzi huo huku maafisa watakaochaguliwa wakihudumu kwa kipindi cha miaka minne.