Ubelgiji kutambua utaifa wa Palestina

Marion Bosire
2 Min Read
Maxime Prévot

Waziri wa masuala ya kigeni wa Ubelgiji, Maxime Prévot, amesema nchi yake itaitambua Palestina mwezi huu na kuiwekea Israel vikwazo 12 vikali.

Ubelgiji itaitambua rasmi Taifa la Palestina katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) baadaye mwezi huu, kwa mujibu wa tangazo la Waziri Prévot.

“Palestina itatambuliwa na Ubelgiji katika kikao cha UN! Na vikwazo vikali vitawekwa dhidi ya serikali ya Israeli,” Prévot, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu, aliandika kwenye mtandao wa kijamii X mapema Jumanne.

Israel itakabiliwa na vikwazo 12 kutoka kwa Ubelgiji, alisema Prévot, vikiwemo marufuku ya uagizaji wa bidhaa kutoka kwa makazi ya walowezi wa Kiyahudi yaliyo haramu katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, pamoja na kuangaziwa upya kwa sera za ununuzi wa bidhaa na huduma za umma kutoka kwa kampuni za Kiyahudi.

Prévot, ambaye ni mwanachama wa chama cha Christian Democrat cha mrengo wa kati, alisema kuwa Ubelgiji inatoa ahadi hiyo kutokana na janga la kibinadamu linaloendelea Palestina, hasa huko Gaza.

Waziri huyo wa masuala ya kigeni pia alisema kuwa utambuzi huo utafanyika rasmi tu baada ya mateka wa mwisho kuachiliwa kutoka Gaza na “Hamas kutokuwa tena na nafasi yoyote katika usimamizi wa Palestina.”

Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Bart De Wever, kutoka chama cha kitaifa cha Flemish, alisema mwezi uliopita kuwa utambuzi wa Palestina unapaswa kuambatana na masharti madhubuti, kwa mujibu wa shirika la habari la Belga la Ubelgiji.

Mwisho wa Julai, Rais Emmanuel Macron alitangaza kuwa Ufaransa itatambua taifa la Palestina wakati viongozi wa dunia watakapokutana kwa ajili ya UNGA.

Ufaransa na Saudi Arabia zitakuwa wenyeji wa mkutano kuhusu utambuzi wa Palestina wakati wa UNGA tarehe 22 Septemba. Australia, Kanada, na Uingereza pia zimesema zinapanga kuutambua Palestina mwezi huu, pia kwa masharti fulani.

Hadi kufikia Aprili mwaka huu, takriban nchi 147, sawa na asilimia 75 ya wanachama wa Umoja wa Mataifa, tayari zilikuwa zimetambua taifa la Palestina.

Share This Article