Tuzo za Trace: Mwijaku amtetea Ali Kiba

Kiba hakuhusishwa kama mtumbuizaji na hakushinda tuzo ya Trace kwenye hafla iliyoandaliwa jana huko Zanzibar.

Marion Bosire
1 Min Read
Ali Kiba

Mtangazaji na mwanaharakati wa mitandaoni nchini Tanzania Burton Mwemba maarufu kama Mwijaku sasa anamtetea msanii wa muziki nchini humo Ali Kiba kuhusiana na tuzo za jana za Trace.

Kupitia akaunti yake ya Instagram Mwijaku amesema, “Trace Awards mnafaa kujitathmini kuhusu mnavyochukulia wasanii mnaoalika kwenye tuzo zenu.”

Hakutaja mara moja alichofanyiwa msanii huyo wa muda mrefu wa muziki wa Bongo Fleva lakini aliendelea kusema kwamba wakati ujao hawataruhusu wasanii kubebwa vibaya.

“Mnatakiwa mtambue kwamba Ali Kiba ni msanii mkubwa Afrika na hampaswi kupepesa macho.” alimalizia mtangazaji huyo wa kituo cha redio cha Crown kinachohusishwa na Ali Kiba.

Kabla ya hapo alikuwa amemshauri Kiba kupitia akaunti yake ya Instagram awafute kazi wanaomsimamia kama msanii lakini pia hakutoa sababu.

“Nasema hivi, usimamizi wa Ali Kiba, kama ningekuwa na uwezo ndani ya King’s Music, wote wangeachishwa kazi mara moja, hawafai kwa kila kitu.” aliandika Mwijaku.

Kiba alikuwa ameteuliwa kuwania tuzo ya Trace katika kitengo cha msanii bora wa Tanzania pamoja na Mbosso, Diamond Platnumz, Zuchu, Marioo, Jux, Harmonize na Nandy aliyeibuka mshindi.

Mmiliki huyo wa kampuni ya muziki ya King’s Music hakuwa kwenye orodha ya waliotumbuiza kwenye hafla ya kugawa tuzo hizo za Trace kisiwani zanzibar.

Share This Article