Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA nchini Tanzania Tundu Lissu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu ambapo mahakama hiyo itatoa uamuzi kuhusu kesi inayomkabili ya uhaini.
Kikao cha leo kinatarajiwa kutoa mwelekeo wa iwapo mashahidi a kesi hiyo watafichwa au kuonyeshwa mubashara kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.
Mahakama pia inatarajiwa kutoa fursa kwa upande wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kumsomea maelezo ya mashahidi na vielelezo ili kesi hiyo inayomkabili iweze kuhamishiwa Mahakama Kuu na kuanza kusikilizwa.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu wa kukubali mashahidi ambao ni raia katika kesi hiyo kufichwa ili kulinda usalama wao.
Mnamo Agosti 13,2025 Wakili wa serikali Mkuu Nassoro Katuga alikumbusha mahakama juu ya uamuzi wa mahakama kuu uliotolewa Agosti 4, ambao ulitoa amri mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari kutoruhusiwa kutangaza mubashara taarifa za mashahidi ambao ni raia na ushahidi wakati wa kusikilizwa kwa kesi.
Lissu amekuwa kizuizini tangu alipokamatwa kwa mara ya kwanza Aprili 9, 2025, kufuatia matamshi aliyotoa jijini Dar es Salaam Aprili 3, 2025.
Kando na madai ya uhaini, Lissu anakabiliwa pia na kesi nyingine ya kuchapisha taarifa zisozo za kweli, makosa yote yakitokana na kampeni aliyokuwa akiongoza ya “No reforms No elections” iliyolenga kuchochea mabadiliko fulani kabla ya uchaguzi mkuu.
Tanzania itaandaa uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025.