Rais William Ruto amesema Kenya iko tayari kuandaa fainali za nane za Kombe la CHAN kati ya Agosti 2 na 30 mwaka huu.
Rais amesema haya leo Jumatano alipozuru uwanja wa kimataifa wa Kasarani, kuukagua baada ya kukamilika kwa ukarabati tayari kwa kipute hicho.
“Leo tunajivunia kusema tutaandaa CHAN kuanzia Agosti 3,” alisema Ruto aliyeandamana na Mawaziri Salim Mvurya wa Michezo na Soipan Tuya wa Ulinzi miongoni mwa maafisa wengine serikalini.
Baadaye, Rais alitembelea kambi ya mazoezi ya timu ya taifa Harambee Stars pembezoni mwa uwanja huo wa Kasarani.
Alitoa hakikisho la kuiunga mkono na kuisaidia Harambee Stars kwa hali na mali kuhakikisha inasajili matokeo bora.

Ruto ametoa changamoto kwa timu hiyo kusajili matokeo bora na kuwafurahisha Wakenya wakati wa fainali hizo za CHAN.
“Tuna imani nanyi; tunawaamini. Tunaamini uwezo wenu na tutawashabikia ili mpate ushindi.”
Makala ya nane ya CHAN yatang’oa nanga Agosti 2 kwa mechi ya kundi B kati ya wenyeji wenza Tanzania -Taifa Stars dhidi ya Burkina Faso uwanjani Mkapa, kabla ya Kenya kukabana koo na DR Congo tarehe 3 katika kundi B katika uwanja wa Kasarani.
Uganda Cranes, ambao pia ni wenyeji wenza, watapimana ubabe na Algeria katika mchuano wa kundi C Agosti 4.