Trump kuzungumza na viongozi wa Urusi na Ukraine kutafuta mwafaka wa kusitisha vita

Alisema hayo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social Jumamosi akielezea matumaini kwamba mazungumzo hayo ya kesho Jumatatu yatafanikiwa.

Marion Bosire
2 Min Read
Donald Trump - Rais wa Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba atazungumza na wenzake wa Urusi na Ukraine pamoja na nchi za NATO kutafuta mwafaka wa kusitisha vita nchini Ukraine.

Alisema hayo kupitia ujumbe aliochapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social Jumamosi akielezea matumaini kwamba mazungumzo hayo ya kesho Jumatatu yatafanikiwa.

“Natumai kwamba itakuwa siku ya mafanikio, mpango wa kusitisha vita utaafikiwa na vita hivi, vita ambavyo havikustahili kuwa vitaisha,” aliandika Trump.

Usemi wa Rais Trump unajiri siku moja baada ya mazungumzo ya kwanza kati ya Russia na Ukraine ya siku tatu kukosa kuafikia mkataba wa kusitisha mapigano.

Rais wa Urusi Vladmir Putin alikosa kufika kwenye majadiliano hayo ambapo alikuwa amealikwa na mwenzake wa Ukraine Volodymr Zelenskyy, na badala yake akatuma ujumbe wa kumwakilisha.

Hatua yake ilimfanya Zelenskyy aseme kwamba hachukulii kwa uzito juhudi za kutafuta amani.

Kilichoafikiwa katika mazungumzo hayo ni kubadilishana wafungwa wa vita 1,000 kila upande na waziri wa ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov aliongeza kwamba hatua itakayofuata ni mkutano kati ya Zelenskyy na Putin.

Jumamosi msemaji wa afisi ya Rais wa Urusi Dmitry Peskov alisema kwamba hatua hiyo inawezekana lakini itakuwa jibu baada ya kazi na baada ya kuafikiwa kwa mambo kadhaa ya makubaliano kati ya pande mbili.

Peskov alisema pande hizo ni lazima kwanza zikamilishe mpango wa kubadilishana wafungwa kabla ya kuandaa raundi nyingine ya mazungumzo.

Mkuu wa ujasusi katika jeshi la Ukraine Kyrylo Budanov, alisema mpango huo wa kubadilishana wafungwa utatekelezwa mapema wiki ijayo.

Mapema Jumamosi, shambulizi wa Urusi la droni katika eneo la Sumy nchini Ukraine lilisababisha vifo vya abiria 9 waliokuwa kwenye basi huku wengine saba wakijeruhiwa.

Share This Article