Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa Israel haiwezi kukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, kauli ambayo inamuweka kwenye mvutano wa moja kwa moja na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na wanachama wa serikali yake ambao wamekuwa wakishinikiza hatua hiyo dhidi ya ardhi ya Wapalestina.
Trump alitoa kauli hiyo ya kushangaza alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi, kabla ya kuwasili kwa Waziri Mkuu Netanyahu nchini Marekani ili kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York leo Ijumaa.
“Sitairuhusu Israel kukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi. Hapana. Sitairuhusu. Haitatokea,” Trump alisema.
Alipoulizwa iwapo alikuwa amezungumza na Netanyahu kuhusu mpango wake wa kuzuia jaribio lolote la Israel kuteka rasmi ardhi hiyo, Trump hakutoa jibu la moja kwa moja.
“Ndiyo, lakini sitairuhusu. Iwe nimezungumza naye au la, sitairuhusu Israel kukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi. Imekwishatosha. Ni wakati wa kusitisha sasa, sawa?” Rais huyo wa Marekani alisema.
Trump hakueleza kwa kina ni hatua gani angechukua kuzuia uwezekano wa Israel kukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, na wachambuzi walitilia shaka iwapo kiongozi huyo wa Marekani mwenye msimamo wa kubadilika-badilika ataendelea kusimamia msimamo huo.
Kauli ya Trump huenda ikaweka serikali yake kwenye mgongano na serikali ya mrengo mkali wa kulia ya Israel inayoongozwa na Netanyahu, ambayo baadhi ya wanachama wake wameifanya sera ya kuikalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi na Gaza kuwa ajenda rasmi ya kisiasa.