Rais wa Amerika Donald Trump, ametaja kuchaguliwa kwa Papa Mtakatifu ambaye ni raia wa Marekani Robert Francis Prevost kuwa heshima kubwa kwa taifa hilo, akidokeza kuwa anatazamia kukutana na Papa huyo ambaye atajulikana kama Leo XIV.
Trump ni miongoni mwa wanasiasa wengi wa Marekani, ambao wamempongeza Papa huyo mwenye umri wa miaka 69 mzaliwa wa Chicago kuliongoza Kanisa Katoliki.
“Kuwa na Baba Mtakatifu kutoka Marekani ni heshima kubwa,” alisema Rais Trump.
Papa Leo XIV alizaliwa Chicago na kuhudhuria Chuo Kikuu cha Philadelphia,kabla ya kunza umishenari huko Peru.
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, ambaye ni mfuasi wa dini ya Katoliki, pia alimpongeza Baba Mtakatifu Leo XIV, kwa kuchaguliwa kuliongoza kanisa Katoliki.
“Nina hakika mamilioni ya wafuasi wa kanisa katoliki Marekani na Wakristo wengine watamuombea awe na ufansi anapoliongoza Kanisa Katoliki,” alisema Makamu huyo wa Rais kupitia ukurasa wake wa X.
Marekani ni ya nne kwa kuwa na idadi kubwa ya waumini wa kanisa Katoliki.