Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani imeweka viwango vipya vya ushuru kwa bidhaa zinazoingia humo kutoka Mexico, Canada na China.
Jumamosi Trump alitia saini maagizo matatu tofauti yaliyoweka ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa za Canada na Mexico na asilimia 10 kwa bidhaa za China.
Hata hivyo bidhaa za nishati kutoka Canada kama mafuta, gesi asilia na umeme zitatozwa ushuru wa asilimia 10.
Trump alisema ushuru huo ni muhimu ili kulinda raia wa Marekani na aliahidi kuudumisha hadi wakati kile anachokitaja kuwa dharura kitakapofikia kikomo nchini Marekani kuhusu dawa ya fentanyl na uhamiaji usiosajiliwa.
Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum naye aliagiza ushuru wa kulipiza kisasi huku waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau akisema nchi yake itaweka viwango sawa vya asilimia 25 vya ushuru kwa bidhaa za thamani ya dola bilioni 155 zinazoagiwa kutoka Marekani.
China haikujibu mara moja.
Wakazi wa jiji la Detroit, lililo karibu na mpaka wa Mexico na raia wa Canada wana hofu kuhusu hatua ya Marekani huku wataalamu wa masuala ya uchumi wakionya kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa vita vya kibiashara.
Iwapo hilo litafanyika basi bei za bidhaa zitapanda mara dufu na kusukuma Canada kwa hali ya kushuka kwa uchumi.
Hatua ya Trump ya Jumamosi ilitekeleza vitisho alivyotoa wakati wa kampeni ya mwaka 2024 na amesusia kabisa ushauri wa wataalamu wa uchumi.
Kulingana na agizo la maandishi la Trump, viwango hivyo vipya vya ushuru vitaanza kukusanywa usiku wa manane Jumanne kulingana na saa za Marekani.
Bidhaa ambazo zimepakiwa na kusafirishwa kabla ya wakati huo zitaepushiwa viwango hivyo vipya vya ushuru.