Trump asisitiza azma ya Marekani kununua Gaza

Trump alisema Gaza inafaa kuchukuliwa kuwa eneo kubwa la ujenzi wa nyumba.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Marekani Donald Trump amesisitiza kuhusu pendekezo lake la kudhibiti ukanda wa Gaza akisema taifa lake limejitolea kununua na kumiliki eneo hilo lililokumbwa na vita.

Akizungumza na wanahabari jana Jumapili ndani ya ndege rasmi ya Rais wa Marekani almaarufu ‘Air Force One’, Trump alisema kwamba Gaza inafaa kuchukuliwa kuwa eneo kubwa la ujenzi wa nyumba.

Trump aliyekuwa akielekea New Orleans kuhudhuria Super Bowl alisema pia kwamba nchi za Mashariki ya kati zinaweza kutwikwa jukumu la kujenga tena Gaza, chini ya uangalizi wa Marekani.

“Lakini tumejitolea kuimiliki, kuichukua na kuhakikisha kwamba Hamas hawarejei humo. Hakuna cha kurejelea huko. Eneo zima ni la ubomozi.” alisema Trump.

Kuhusu Wapalestina waliopoteza makazi yao huko Gaza, Trump anahisi kwamba hawangependelea kurejea huko, hata ingawa pendekezo lake limekashifiwa na viongozi wa wapalestina na wengine wa ulimwengu.

Anapendekeza watu hao wapatiwe makazi mbadala katika eneo salama akifafanua kwamba wanataka kurejea Gaza kwa sababu hawana eneo lingine la makazi.

Kundi la kipalestina la Hamas, linalodhibiti Gaza linapinga mapendekezo ya Trump na limeyataja kuwa upuuzi.

“Gaza sio mali ambayo inaweza kuuzwa na kununuliwa na ni sehemu muhimu ya ardhi ya makazi ya Palestina.” alisema Izzat al-Risheq, wa kundi linalotawala kisiasa la Hamas kwenye Telegram.

Anahisi kwamba kushughulikia matatizo ya Gaza kwa kutumia fikra za mtu anayejihusisha na ujenzi na uuzaji wa nyumba ni ishara ya kuambulia patupu.

Al-Risheq alisema pia kwamba wapalestina watakomesha mipango ya kuwahamisha akisema eneo la Gaza linamilikiwa nao.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa upande mwingine amefurahikia pendekezo la Trump ambalo analitaja kuwa la mabadiliko na bunifu.

Share This Article