Rais Donald Trump amewasilisha ombi la dharura katika Mahakama ya Juu ya Marekani ili iamue ikiwa ana mamlaka ya kumfukuza kazi mmoja wa viongozi waandamizi serikalini, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani.
Hampton Dellinger, Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Mwanasheria Maalumu, amemshtaki Trump baada ya kufutwa kazi kupitia baruapepe mwezi huu.
Trump pia amewafukuza wakaguzi wakuu kadhaa katika mashirika mbalimbali ya serikali pamoja na maelfu ya wafanyakazi wa serikali ya Marekani.
Bw. Dellinger, aliyeteuliwa na rais wa zamani Joe Biden, anasema kufutwa kwake kunakiuka sheria inayowalinda viongozi wa mashirika huru dhidi ya kufutwa kazi na rais, “isipokuwa katika kesi za uzembe wa kazi, matumizi mabaya ya madaraka, au kutoendana na majukumu yao”.
Jaji wa shirikisho mjini Washington DC alitoa amri ya muda Jumatano inayomruhusu Dellinger kuendelea na kazi yake huku kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa.