Mwanamuziki wa mtindo wa Rap wa asili ya Canada Daystar Peterson maarufu kama Tory Lanez anaripotiwa kuwa katika hali dhabiti hospitalini baada ya kuchomwa kisu gerezani.
Lanez anahudumia kifungo kilichotokana na kesi ya kumpiga risasi mwanamuziki mwenza Megan Thee Stallion mwaka 2020. Amekuwa akizuiliwa katika gereza la California ambapo kisa hicho kilitokea.
Mfungwa mwenzake anaripotiwa kumchoma kisu cha kujitengenezea walipokuwa nje na akakimbizwa kwenye hospitali iliyo karibu Jumatatu asubuhi kulingana na saa za Marekani.
Baadaye chapisho kwenye akaunti ya Lanez ya Instagram lilithibitisha kwamba alidungwa kisu mara 14, mara saba mgongoni, mara nne kwenye tumbo na kifua, mara mbili nyuma ya kichwa na mara moja katika sehemu ya kushoto ya uso wake.
Taarifa hiyo ilielezea kwamba mapafu yake yaliathirika ikabidi akawekewa vifaa vya kumsaidia kupumua lakini baadaye viliondolewa na anapumua vizuri.
“Hata ingawa ana maumivu, anazungumza kama kawaida na anashukuru mungu kwamba anapata nafuu” alisema taarifa hiyo.
Lanez amekuwa akitumikia kifungo cha miaka 10 gerezani tangu Agosti 2023 alipopatikana na hatia zinazohusiana na matumizi ya silaha aina ya bunduki.
Januari mwaka huu, mahakama ilimpa Megan agizo la kuzuia Lanez kuwasiliana naye baada ya kudai kwamba alikuwa akimsumbua hata kutoka gerezani.