Tina Knowles azungumzia video inayomwonyesha akizomea Rumi

Walikuwa jukwaani wakati wa tamasha la Beyonce ambapo alikuwa anamtambulisha huku Rumi akimvuta kwa lengo la kuchukua kipaaza sauti.

Marion Bosire
2 Min Read
Tina Knowles

Mamake mwanamuziki Beyonce Tina Knowles amezungumzia video iliyosambaa mitandaoni inayomwonyesha akizomea mjukuu wake Rumi ambaye ni binti ya Beyonce wakiwa jukwaani wakati wa onyesho la Beyonce.

Katika video hiyo iliyonakiliwa wakati wa onyesho la kimuziki la Beyonce kama sehemu ya ziara yake ya Cowboy Carter, Tina alionekana akimzomea Rumi ambaye alikuwa akijaribu kumshika mamake aliyekuwa akizungumza.

Beyonce alikuwa anamtambulisha mamake kwa umati uliokuwepo akimsifia kwani kitabu chake ambacho anaendelea kutangaza kimepata mauzo ya kiwango cha juu.

Rumi wa umri wa miaka 7, kama mtoto wa kawaida ambaye pia alikuwa na furaha ya kuwa jukwaani na mamake alijaribu kumshika lakini Tina hakumruhusu.

Baadaye Blue Ivy kifungua mimba wa Beyonce wa umri wa miaka 13, alimchukua Rumi akasimama karibu naye huku akimnyamazisha.

Katika mahojiano na Gayle King hivi maajuzi, Tina alisema kwamba alichukua hatua ya kumzomea Rumi kutokana na hofu kwamba angempokonya mamake kipaaza sauti.

Aliongeza kwamba Rumi alitaka kuzungumza siku hiyo lakini alikuwa anavuta kwa nguvu na kipaanza sauti kingeanguka na kumgonga uso.

Hata hivyo alisema kwamba alifurahia kuwa jukwaani na binti yake pamoja na wajukuu zake siku hiyo.

Tina aliandika kitabu kiitwacho “Matriarch” ambacho anaendelea kutangaza kwenye vyombo vya habari huku kikiripotiwa kuafikia mauzo ya kiwango cha juu.

Share This Article