Timu ya kupambana na ufisadi yapigwa breki na mahakama

Martin Mwanje
2 Min Read

Mahakama Kuu ya Milimani meizuia Timu yenye Asasi Mbalimbali Iliyobuniwa Kupambana na Ufisadi nchini (MAT) dhidi ya kuanza kutekeleza majukumu yake. 

Kesi ya kupinga kubuniwa kwa timu hiyo iliwasilishwa kwenye mahakama hiyo na Dkt. Magare Gikenyi, Eliud Matindi na watu wengine wawili waliofika mbele ya Jaji Bahati Mwamuye.

Wote hao wanadai Rais hana mamlaka ya kubuni timu kama hiyo.

Mahakama imetoa agizo ka kuizuia timu hiyo kuanza kuchapa kazi hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Jana Jumanne, Rais Ruto alibuni timu hiyo kwa lengo la kuimarisha jitihada za kupambana na jinamizi la ufisadi nchini.

Timu hiyo pia imekabidhiwa jukumu la kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa kiuchumi na makosa mengine husika.

MAT italeta pamoja asasi mbalimbali ikiongozwa na Ofisi Kuu ya Rais huku Katibu wake akiwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu.

Asasi zingine kwenye timu hiyo ni Idara ya Taifa ya Ujasusi (NIS), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini (EACC), Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Kituo cha Kuripoti Masuala ya Fedha (FRC).

Mamlaka ya Kutwaa Mali Iliyopatikana Kinyume cha Sheria (ARA), Mamlaka ya Kukusanya Mapato (KRA), Benki Kuu nchini (CBK) na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) pia zimejumuishwa kwenye timu hiyo.

Timu hiyo imepewa jukumu la kuongeza asasi zingine zinazoweza kuboresha utenda kazi wake.

“MAT, kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo, itakuza ushirikiano na uratibu ili kuboresha ufanisi wake katika vita dhidi ya ufisadi. Kwa lengo hili, timu hiyo itafadhiliwa na mgao wa fedha wa asasi wanachama na vyanzo vingine vya fedha,” alisema Rais Ruto kwenye taarifa jana Jumanne.

Timu hiyo ilibuniwa wakati ambapo kiongozi wa nchi amezituhumu kamati za bunge kwa kuwa na hulka ya kuitisha hongo kutoka kwa watu wanaofika mbele yake.

Amelitaka bunge kukomesha hulka hiyo anayosema ni tishio kwa mustakabali wa taifa.

Share This Article