Timu ya Kenya kuondoka leo kwenda China kwa mbio za kupokezana kijiti duniani

 Kenya itashiriki katika fani za mita 400 kupokezana kijiti kwa wanaume na wanawake, mita 400 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti mseto na mita 100 kwa wakimbiaji wanne kupokezana kijiti.

Dismas Otuke
1 Min Read

Timu ya Kenya inatarajiwa kuondoka nchini leo jioni kuelekea Guangzhou, China, kushiriki makala ya saba ya mbio za kupokezana Kijiti Duniani kati ya tarehe 10 na 11 mwezi huu.

Wanariadha wa Kenya wamekuwa kwa kambi ya mazoezi kwa takriban majuma matatu katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex, kujiandaa kwa mashindano hayo.

Bingwa wa jumuiya ya madola katika mita 100 Ferdinand Omanyala, ataongoza kikosi cha mita 100 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti kinachomshirikisha kakake mdogo Isaac Omurwa, Meshack Babu, Mark Otieno, Steven Oyango na Moses Wasike.

Kulingana na kocha Stanley Towet, wanalenga sio tu medali huko China, ila kikubwa zaidi ni kutimiza muda wa kufuzu kwa mashindano ya Riadha ulimwenguni mwezi Septemba mwaka huu mjini Tokyo, Japan.

Hata hivyo, kikosi cha Kenya, hususan timu ya mita 400 kwa wanariadha wanne, kupokezana kijiti mseto, na ile ya wanawake  ya mita 400,zimepatwa na pigo kufuatia kujiondoa kwa bingwa wa dunia wa mita 800 Mary Moraa,  aliyekosa viza.

Kenya itashiriki katika fani za mita 400 kupokezana kijiti kwa wanaume na wanawake, mita 400 kwa wanariadha wanne kupokezana kijiti mseto na mita 100 kwa wakimbiaji wanne kupokezana kijiti.

Share This Article