Msanii wa muda mrefu wa muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania Khalid Mohamed maarufu kama TID(Top In Dar es Salaam) ametoa maoni yake kuhusu uimbaji wa moja kwa moja wa kutumia bendi.
TID alikuwa akijibu maswali ya wanahabari kuhusu kisa cha hivi maajuzi kilichofichua kwamba wasanii wengi wa Tanzania hawawezi kuimba moja kwa moja jukwaani kwa kutumia bendi.
Alitakiwa kutoa maoni kuhusu kinachosababisha hali hiyo iliyoshuhudiwa kwenye tamasha la kutoa tuzo za Trace kisiwani Zanzibar Februari 26, 2025.
Kulingana naye, wasanii kama hao hawajafanya mazoezi ya kutosha ya uimbaji, “Hawaja practice, mtu anataka kuwa msanii tu anaenda studio anaimba anajiita yeye msanii.”
Alishangaa wasanii kama hao hawajui hata sauti wanazoimba huku akitoa mfano kwamba yeye amepiga mazoezi miaka mingi na anajua anaimba ‘C Major’ au ‘D – Minor’.
Msanii huyo amehimiza wanamuziki wafanye mazoezi ya sauti na hata wajiunge kwenye shule za muziki na wala sio tu kwenda studioni kurekodi nyimbo.
Suala la wasanii wa Tanzania kutokuwa na uwezo wa kutumbuiza moja kwa moja kwa kutumia bendi limezua mjadala mitandaoni, baada ya wengi wa waliotumbuiza kwenye Trace awards kushindwa kuimba vizuri.
Walionekana wenye mazoea ya kutumia nyimbo walizorekodi kutumbuiza katika matamasha, huku msanii wa Kenya Bien Barasa akifanya vyema na kuridhisha wengi wa waliohudhuria.