Mwanamuziki wa Nigeria Teniola Apata maarufu kama Teni amelazimika kukana maneno yake mwenyewe kama yalivyo kwenye wimbo wake Money.
Hii ni baada ya mwimbaji huyo ambaye pia hurejelewa kama Sugar Mummy of Lagos kuuga kwa muda kiasi cha kulazwa hospitalini.
Kwenye wimbo huo wake, Teni anasema, wanasemapesa haziwezi kununua furaha, haziwezi kununua mapenzi, haziwezi kujaza utupu moyoni, lakini anataka pesa zote ulimwenguni.
Anaendelea kuimba kwamba ni heri alilie kwenye gari la kifahari aina ya Bentley, akinywa Hennessy huku akifuta machozi kwa kutumia noti za dola 100.
Teni alichapisha video inayomwonyesha akishughulikiwa na madaktari na kuandika, “Pesa haziwezi kukununulia afya, ni Mungu.”
Lakini msanii huyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu kinachomsibu kiafya.
Tarehe 14, mwezi Februari mwaka huu wa 2025, aligonga vichwa vya habari ndani na nje ya Nigeria kutokana na hatua yake ya kusaidia mama mmoja mchuuzi.
Alimtoa kwenye kibanda chake cha kuuzia vitu nje ya eneo moja la makazi, akampeleka akatengenezwa nywele, akamnunulia mavazi mapya na kisha kumpa mtaji wa Naira Milioni moja.
Alimfaa pia mama mwingine ambaye alirekodiwa video na wanawe akiimba wimbo wa ‘Money’ kwa weledi mkubwa ambapo alimnunulia bidhaa za kutumia nyumbani kisha akampa hela pia.