Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Ulanga, mkoani Morogoro Christopher Bwakila amemhukumu kifungo cha miaka 30 jela na faini ya sh 500,000 ambazo ni sawa na shilingi 25,000 fedha za Kenya, Antony Elias Myonga kwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la tatu.
Myonga ambaye ni mkazi wa Ubuyu, imetajwa alitenda kosa hilo Agosti 10 mwaka huu ambapo alikwenda Mahenge mjini kwa ajili ya kuuza mahindi na baada ya biashara yake kumalizika alishindwa kurudi mashambani kutokana na muda na kuomba hifadhi nyumbani kwa bibi anayeishi na wajukuu zake wawili wakike mmoja mwenye umri wa miaka 11, mwanafunzi wa darasa la 3 na mwengine mdogo ambaye bado hajaanza kusoma.
Bibi huyo mwenye undugu na mshtakiwa, alimkaribisha na kumruhusu kulala sebuleni huku chumba kimoja akilala yeye na kingine wakilala wajukuu zake.
Aidha,Kabla ya kulala Mshtakiwa alipata muda wa kuzungumza na binti ambaye anafahamiana naye kama ndugu yake kitendo ambacho kilisababisha kumuomba fedha sh 2000 ambazo ni sawa na shilingi 100 fedha za Kenya na mtuhumiwa kumpa masharti ya kukutana naye kimwili ndipo apewe pesa hizo.
Ilipofika majira ya usiku wa manane Mshtakiwa alitoka sebuleni na kwenda chumbani kwa binti na kumbaka mbele ya mdogo wake huku akipiga kelele kwa maumivu kiasi kilichosababisha bibi yao kuamka na kwenda kumsaidia binti na ndipo Mshtakiwa alipopata nafasi ya kutoroka na kuelekea pasipojulikana hadi alipokamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa Mahakama.