Tamasha la Alien Skin lafutiliwa mbali

Tamasha hilo lingeandaliwa Februari 21, 2025 katika hoteli ya Africana.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Alien Skin amethibitisha kufutiliwa mbali kwa tamasha lake lililokuwa likisubiriwa kwa hamu ambalo lingeandaliwa Februari 21, 2025 katika hoteli ya Africana.

Rais huyo wa kampuni ya muziki ya The Fangone Forest alitangaza hayo kupitia mitandao ya kijamii akisema kwamba aliafikia uamuzi huo kufuatia shinikizo za maadui na wala sio uamuzi wa usimamizi wa hoteli ya Africana.

Katika taarifa yake, Alien Skin alidhihirisha kukatizwa tamaa kwa kile alichokitaja kuwa upendeleo dhidi ya maendeleo yake kama msanii.

Alionekana kuashiria kwamba maafisa wa usalama wanaogopa ushawishi wake na umati mkubwa wa mashabiki ambao huwa anavutia.

Huku akisisitiza kulengwa kwa tamasha lake visivyo, wasiwasi uliibuliwa pia kuhusu usalama kufuatia visa kadhaa vya vurugu vinavyohusishwa naye na marafiki zake.

Ameahidi kutafuta eneo jingine la kuandaa tamasha na atajuza mashabiki zake baadaye.

Alien Skin ambaye jina lake halisi ni Patrick Mulwana amehusishwa na visa kadhaa vya vurugu nchini Uganda hasa mwanzo wa mwaka huu kwenye matamasha ya kukaribisha mwaka mpya.

Mojawapo ya visa hivyo vilitokea kwenye tamasha la Empelle huko Buloba ambapo yeye na kundi lake waliingia jukwaani kwa lazima mwanamuziki Palasso akiendelea kutumbuiza.

Hatua hiyo ilisababisha mvutano kati ya mashabiki wa wawili hao na baadaye Palasso na kundi lake wakavamia makazi ya Alien Skin kulipiza kisasi.

Share This Article