Talanta FC na Nairobi City Stars zimeondolewa kwenye Ligi Kuu ya Kenya, baada ya kumaliza katika nafasi mbili za mwisho msimu wa mwaka 2024 na 2025 uliokamilika Jumapili.
City Stars wamemaliza nafasi ya mwisho kwa alama 35, baada ya kutoka sare tasa na Mathare United, huku Talanta ikipigwa goli moja kwa bila na Murang’a Seal walionusurika.
Posta Rangers iliyomaliza ya 16 itamenyana na Naivas FC, iliyomaliza ya tatu katika ligi ya NSL kataika mechi ya mikondo miwili huku mshindi akicheza ligi kuu msimu wa mwaka 2025/2026.
Police FC wametawazwa mabingwa baada ya kutoka sare ya bao moja na Gor Mahia, katika mechi ya mwisho wakifunga msimu kwa pointi 65, wakifuatwa na Gor kwa alama 59.
Kakamega Homeboyz iliyotoka sare tasa dhidi ya Tusker FC ,ni ya tatu kwa alama 58, moja zaidi huku Tusker wakishikilia nafasi ya nne kwa pointi 56, nao Shabana FC ,wanakamilisha tano bora kwa alama 53.
Police FC wataiwakilisha Kenya katika kombe la Ligi ya mabingwa Afrika msimu ujao .
Mwakilishi wa pili wa Kenya kwa mashindano ya Afrika atabainika wakati wa fainali ya kombe la Mozzartbet kati ya Gor na Nairobi United.