Tahadhari yatolewa dhidi ya dawa ghushi ya kutibu saratani

Tom Mathinji
1 Min Read
Dawa aina ya Avastin.

Bodi ya Dawa na Sumu hapa nchini (PPB), imetoa tahadhari kuhusu dawa ghushi ya inayodaiwa kutibu saratani ambayo inasambazwa hapa nchini.

Kupitia kwa taarifa, bodi hiyo imesema shehena ya dawa ghushi aina ya Avastin (Bevacizumab miligramu 100) ina chanjo yenye nambari H0573B01, inadaiwa kutengenezwa na kampuni ya kimataifa ya dawa ya Roche.

Bodi hiyo imeonya kuwa dawa hiyo ghushi ni hatari kwa wagonjwa wanaotegemea Avasti kudhibiti makali ya saratani ya utumbo, mapafu na figo.

Bodi huiyo imezishauri hospitali, maduka ya kuuzia dawa na wauzaji dawa kukagua shehena waliyo nayo na kuripoti kwa dharura shehena wanazoshuku zina dawa hizo ghushi.

Bodi hiyo inafanya kazi na mashirika ya upelelezi ili kuwanasa wanaoeneza dawa hiyo.

Wakati huohuo bodi hiyo ilitoa wito kwa wahusika katika sekta ya afya kununua bidhaa za matibabu kutoka kwa watengenezaji na wasambazaji bidhaa walioidhinishwa.

“Ununuzi wa bidhaa za matibabu kutoka kwa wasambazaji ambao hawajaidhinishwa unahatarisha maisha ya mgonjwa na utasababisha kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria,” ilisema bodi hiyo.

Share This Article