Syria yaondoa wapiganaji wa Bedouin jijini Suwayda

Tangazo hilo la Jumamosi lilijiri baada ya Rais wa Syria, Ahmed al-Sharaa, kuamuru kusitishwa kwa mapigano kati ya makundi ya Bedouin na Druze.

Marion Bosire
3 Min Read

Serikali ya Syria imesema imeondoa wapiganaji wa kabila la Bedouin kutoka mji wa Suwayda ambao wengi wa wakazi wake ni watu wa jamii ya Druze.

Syria imetangaza pia kusitishwa kwa mapigano ya umwagaji damu katika eneo hilo, saa chache baada ya kupeleka vikosi vya usalama katika eneo la kusini lililojaa machafuko.

Tangazo hilo la Jumamosi lilijiri baada ya Rais wa Syria, Ahmed al-Sharaa, kuamuru kusitishwa kwa mapigano kati ya makundi ya Bedouin na Druze.

Hii ni baada ya makubaliano mengine yaliyosimamiwa na Marekani kwa lengo la kuzuia kuingilia zaidi kwa jeshi la Israel katika mzozo huo.

Kabla ya tangazo hilo la serikali, kulikuwa na ripoti za milio ya risasi katika mji wa Suwayda na mashambulizi ya mizinga katika vijiji vya karibu.

Hakukuwa na ripoti za majeruhi au vifo.

Nour al-Din Baba, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria, alisema katika taarifa kuwa mapigano yalikoma baada ya juhudi kubwa za kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano na kupelekwa kwa majeshi ya serikali katika maeneo ya kaskazini na magharibi mwa mkoa wa Suwayda.

Alisema mji wa Suwayda, magharibi mwa mkoa huo, sasa umesafishwa na hawapo tena wapiganaji wa kikabila na mapigano ndani ya vitongoji vya mji huo yamekoma.

Mapigano hayo yalianza wiki iliyopita baada ya kutekwa kwa dereva wa lori wa jamii ya Druze kwenye barabara kuu, jambo lililosababisha msururu wa mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Hali hiyo ilivutia wapiganaji wa kikabila kutoka maeneo mbalimbali ya nchi waliokuja kuunga mkono jamii ya Bedouin iliyoko Suwayda.

Mapigano hayo yaliwahusisha pia wanajeshi wa serikali ya Syria.

Israel iliingilia kati mzozo huo Jumatano kwa kufanya mashambulizi makali ya anga dhidi ya Suwayda na mji mkuu wa Syria, Damascus, ikidai kuwa ilikuwa inalinda jamii ya Druze baada ya viongozi wa jamii hiyo ndogo kuishutumu serikali kwa ukiukaji dhidi yao.

Watu wasiopungua 260 wameuawa katika mapigano hayo, na wengine 1,700 wamejeruhiwa, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Syria. Hata hivyo, makundi mengine yanaweka idadi ya waliouawa kuwa zaidi ya 900.

Zaidi ya watu 87,000 pia wamelazimika kuhama makazi yao.

Mapigano haya ni changamoto ya hivi karibuni kwa serikali ya al-Sharaa, ambayo ilichukua madaraka baada ya kumuondoa madarakani Rais Bashar al-Assad mwezi Desemba.

Al-Sharaa, katika hotuba ya televisheni Jumamosi, alizitaka pande zote kuweka chini silaha na kushirikiana na serikali kurejesha amani.

Share This Article