Wachezaji wa timu ya taifa ya Nigeria Super Eagles wamesusia mazoezi mjini Rabat, Morocco, wakidai kulipwa marupurupu siku moja kabla ya nusu fainali ya mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka 2026 dhidi ya Gabon.
Wachezaji na maafisa wa benchi ya kiufundi ya Super Eaglkes yamkini wanadai malimbikizi ya marupurupu ya tangu mwaka 2019 pamoja na marupurupu waliyoahidiwa na serikali kwa kufuzu fainali za AFCON mwaka huu na pia kufuzu kwa mechi za mchujo kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Wachezaji na maafisa wa kiufundi walisema wanataka suluhu ya haraka na wamechoka na ahadi hewa za kupokea malipo yao kabla ya kurejelea mazoezi.
Super Eagles watachuana na Gabon kesho Alhamisi Novemba 13 katika nusu fainali ya kufuzu kwa Kombe la Dunia katika uwanja wa Prince Moulay El Hassan Complex mjini Rabat.
Mgomo huo unafuatia madai yaliyoibuliwa awali kuhusu mazingira duni, ikiwemo hoteli chwara ambayo kikosi cha Nigeria kimekodiwa nchini Morocco na shirikisho la NFF kuelekea kwa mechi hizo za mchujo. Mshindi kati ya Nigeria na Gabon atapambana na mshindi wa nusu fainali ya pili baina ya Cameroon na DR Congo katika fainali huku mshindi wa jumla akichuana na timu ya bara jingine.