Mkenya Steve Abdukareem Munyakho hatimaye ameachiliwa huru nchini Saudi Arabia.
Katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje Korir Sing’Oei anasema Munyakho aliachiliwa huru leo Jumanne, majira ya saa nne asubuhi, baada ya kutimiza kikamilifu amri ya Idara ya Mahakama nchini humo.
Munyakho alikuwa amehukumiwa kifo kwa njia kunyongwa nchini Saudia baada ya kupatikana na hatia ya kumuua raia wa Yemen nchini humo mnamo mwezi Aprili mwaka 2011.
Akiwa meneja wa ghala, Munyakho alipigana na Abdul Halim Mujahid Markad Saleh, ambaye familia yake bado inaishi Saudi Arabia..
Wakati wa ugomvi huo, Stephen alimchoma kisu Abdul kwenye paja na kidole gumba. Baadaye Abdul alitembea hadi hospitali ambapo alifariki dunia.
Kufuatia tukio hilo, Munyakho alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la mauaji. Hata hivyo, familia ya Yemeni ilikata rufaa dhidi ya hukumu hiyo katika Mahakama ya Shariah, ikitumia ‘haki ya kulipiza kisasi’.
Munyakho, ambaye alikuwa amefungwa kwa miaka 13, mwanzoni aliratibiwa kunyongwa Mei 15, 2024.
Hata hivyo, mamlaka nchini humo ziliongeza muda hadi Julai 26, 2024, kisha zikaahirisha muda huo kwa miezi minne hadi Novemba 26, 2024.
Munyakho ni mwanawe mwanahabari mkongwe humu nchini, Dorothy Kweyu.