Spika Wetangula atangaza tarehe ya maombi ya kitaifa mwaka 2025

Mkutano huo unaoambatana na kiamsha kinywa utaandaliwa Alhamisi, Mei 29 2025, katika hoteli ya Safari Park, jijini Nairobi.

Marion Bosire
3 Min Read

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ametangaza tarehe ya maombi ya kitaifa ya mwaka huu wa 2025.

Mkutano huo wa kila mwaka unaoambatana na kiamsha kinywa utaandaliwa Alhamisi, Mei 29 2025, katika hoteli ya Safari Park, jijini Nairobi.

“Waheshimiwa Wabunge, kama mnavyofahamu, mkutano wa Kitaifa wa Maombi wa kila mwaka kwa kawaida huandaliwa Alhamisi ya mwisho wa mwezi Mei. Kwa muktadha huu, napenda kuarifu Bunge kuhusu tarehe na ukumbi wa mwaka huu” alisema Spika Wetang’ula.

Maombi hayo ni mkutano wa ibada ya pamoja unaowaleta pamoja viongozi kutoka sekta mbalimbali za jamii kwa ajili ya maombi, tafakari na kujitoa upya kwa taifa.

“Maombi ya Kitaifa ni ibada ya pamoja ya kidini inayoratibiwa na Wabunge, ikiwaleta pamoja viongozi kutoka ndani na nje ya nchi kutafakari, kuomba na kujitoa tena kwa maadili ya utumishi na utaifa” alieleza Spika Wetang’ula.

Mwaka huu, tukio hili litafanyika chini ya kaulimbiu ya ‘Inuka na Ujenge Tena’ wito wa wakati mwafaka kwa umoja wa kitaifa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Kenya.

“Hii ni fursa ya kitaifa ya kutafakari na kuimarisha umoja, hasa katika kipindi ambacho taifa letu linajitafuta upya katika sekta muhimu” alisema Spika Wetang’ula.

Rais wa Jamhuri ya Kenya William Samoei Ruto, atahudhuria hafla hiyo kama Mgeni Mkuu, akisisitiza jukumu kuu la uongozi na kiroho katika safari ya ujenzi wa taifa la Kenya.

“Ili kuwezesha ushiriki wenu, Wabunge wote wanahimizwa kuchukua kadi zao rasmi za mwaliko kwa tukio hilo kutoka mapokezi makuu kuanzia leo” alihimiza Spika Wetang’ula, akionya dhidi ya kuchelewa dakika za mwisho.

Kwa maelezo na mwongozo wa mipango, Wabunge wanaweza kuwasiliana na mbunge Samuel Chepkonga, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya mkutano wa Kitaifa wa Maombi.

Aidha, matukio mawili muhimu ya kabla yamepangwa kufanyika siku ya Jumatano, tarehe 28 Mei 2025, katika ukumbi huo huo. Tukio la kwanza ni Mkutano wa Wanawake, ambao utazingatia kukuza uongozi, ushirikishaji na uwezeshaji wa wabunge wa kike.

“Wabunge wote wanawake wanahimizwa kuhudhuria kikao hiki muhimu” alisema Spika Wetang’ula.

Mkutano wa Kitaifa wa Maombi unasalia kuwa moja ya majukwaa ya kipekee ya kuunganisha taifa kwa mazungumzo ya maadili na tafakari ya kitaifa, ukiongozwa na dhamira ya pamoja ya Bunge kupitia ushirikiano wa vyama vyote na madhehebu mbalimbali.

Share This Article