Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, ametoa wito wa kufanyiwa marekebisho sheria inayodhibiti maandamano, akidokeza kuwa kwa muda wa miaka mingi sheria hiyo imekiukwa.
Wetang’ula alilaani ghasia zilizoshuhudiwa kote nchini ambazo zimesababisha uharibifu wa mali, watu kujeruhiwa na maafa, aalizosema zingeepukwa ikiwa waandalizi wa maandamano hayo wangezingatia sheria.
“Katiba inahakikisha haki ya kuandamana, lakini haitoi ruhusa ya ghasia, wizi, uharibifu wa mali au mauaji. Huu ni ukiukaji wa sheria na haupaswi kuruhusiwa,” alisema Wetang’ula.
Alitoa wito kwa kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah na wabunge wengine, kuongoza mchakato wa kufanyia marekebisho katiba iliyopitishwa mwaka 2010, ili kuziba mianya inayotoa fursa kwa ghasia kwa kisingizio cha maandamano ya amani.
Aliwahimiza Wakenya kukataa kugawanywa kisiasa na kulinda sifa nzuri ya taifa hili.