Uongozi wa Bunge la Taifa umesisitiza kwamba utendakazi, kuhudhuria vikao vya kamati na kuhusika moja kwa moja katika majadiliano vitakuwa vigezo vikuu katika kuunda upya kamati mbalimbali za bunge hilo.
Spika Moses Wetang’ula amesema kamati hizo ni muhimu kwa kazi ya bunge na kusisitiza kwamba wabunge wanaodhihirisha kujitolea, ustadi na uwajibikaji katika majukumu yao watapatiwa kipaumbele katika muundo mpya.
Wetang’ula anamtaka kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah, kiongozi wa wachache Junet Mohamed na viranja wao waharakishe mchakato wa kuunda upya kamati za bunge.
Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kwamba kamati hizo zinaundwa na kulainishwa kuambatana na malengo ya bunge kufikia wakati bunge linarejelea vikao vyake.
Kadhalika, Spika huyo alihimiza wabunge kuchukulia kwa uzito majukumu yao ya kamati za bunge akisisitiza kwamba ufanisi wa bunge unategemea pakubwa kujitolea na utendakazi wa kamati za bunge kwa majukumu yao.
Aliongeza kusema kwamba mchakato wa kuunda upya kamati za bunge unastahili kuzingatia haki na ujumuishaji huku ukidumisha utaalamu na michango ya wanachama binafsi ili kuongeza tija ya bunge.
Haya yanafuatia kukamilika kwa kipindi cha kuhudumu cha kamati za sasa 18 kilichowiana na awamu iliyokwisha. Kamati hizo ni pamoja na ile ya shughuli za bunge, ya mamlaka na fadhila, ya michakato na sheria za bunge na ile ya huduma na vifaa kwa wabunge.
Wetang’ula aliwatia moyo wabunge akisema ana uhakika kwamba hakuna atakayekosa uanachama wa kamati moja au mbili hivi kwani uteuzi utatekelezwa na viongozi wao.
“Tafadhali msizuru afisi ya Spika kumwomba awaweke kwenye kamati fulani kwa sababu hana uwezo wa kufanya hivyo,” Wetang’ula aliambia wabunge.
Ichung’wah kwa upande wake alisema uundaji upya wa kamati za bunge utaashiria uwezo na utaalamu mbali mbali wa wabunge. Alisema pia kwamba wanatambua nafasi zilizoachwa wazi na wabunge waliofanywa mawaziri.
Alisema shughuli ya kujaza nafasi hizo inaendelea na kwamba atatoa habari kuhusu hilo wakati unaofaa na kwamba wataacha nafasi katika kamati mbalimbali kwa wabunge watakaochaguliwa kwenye chaguzi ndogo.
Karani wa bunge Samuel Njoroge alisema kuna mapendekezo mengi ya sheria yanayosubiri kushughulikiwa bungeni akisema mtindo huo unazua wasiwasi.
Kulingana naye, mapendekezo hayo zaidi ya 200 hayajashughulikiwa na kamati husika huku akiwataka wenyeviti wa kamati hizo kuharakisha mchakato wa mapendekezo hayo.