Spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire abanduliwa

Tom Mathinji
1 Min Read
Spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire abanduliwa.

Spika wa bunge la kaunti ya kilifi Teddy Mwambire amebanduliwa rasmi kwenye wadhifa huo na wawakilishi wadi wa bunge hilo.

Mwambire alitimuliwa baada ya wawakilishi wadi 40 kupiga kura ya kuunga mkono mswada wa kumbandua mamlakani, huku wawakilishi wadi 10 wakipiga kura ya kupinga hoja hiyo.

Jumla ya wawakilishi wadi 50 wa bunge hilo wameshiriki zoezi la upigaji kura kuhusu mswada huo wa kuondolewa mamlakani kwa spika huyo.

Mswada wa kumbandua mamlakani Mwamabire uliwasilishwa bungeni humo na mwakilishi wadi ya Tezo Thomas Chengo, ambaye pia ni kiranja wa wachache katika bunge hilo kutokana na madai ya utumizi mbaya wa afisi miongoni mwa sababu nyinginezo.

Chengo pia alimlaumu Spika huyo kwa kuhujumu operesheni za kamati za bunge hilo na kudumaza mchakato wa utayarishaji bajeti ambapo alivunjilia mbali kamati ya bajeti na badala yake kupendekeza kamati ya bunge lote.

Kufuatia hatua hiyo, Naibu Spika wa bunge hilo Naftal Kombo sasa amechukuwa wadhifa wa kaimu spika, ambapo atahudumu kwa muda wa siku 21 hadi spika mpya atakapochaguliwa.

Share This Article