Spice afutilia mbali tamasha nchini Uganda

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa kike wa mtundo wa Dancehall kutoka Jamaica Spice ametangaza kufutiliwa mbali kwa tamasha lake nchini Uganda kufuatia kutoelewana na waandalizi kuhusu mkataba.

Spice alitangaza kufutwa kwa onyesho hilo lililokuwa limepangiwa kuandaliwa Disemba 6, 2025, kupitia akaunti yake ya mtandao wa Facebook.

Katika chapisho hilo lililowavunja moyo mashabiki wake nchini Uganda, Spice alidhihirisha msisimko aliokuwa nao kuhusu tumbuizo hilo lakini akalalamika kwamba halitatimia.

Alisema kwamba alikuwa amejiandaa kikamilifu kwa shughuli hiyo ambayo ni sehemu ya ziara anazofanya katika maeneo mbali mbali ulimwenguni.

Hatua yake ya kujiondoa kwenye tamasha hilo imezua minong’ono mitandaoni ambapo wafuasi wake wameonyesha alivyowavunja moyo wengine wakionyesha kwamba wanaelewa hali ilivyo.

Spice anafahamika kwa kutumbuiza kwa njia ya kipekee jukwaani huku mitindo yake ya mavazi ikiongeza uzuri wa maonyesho yake.

Tumbuizo la Uganda lilitizamiwa kuwa moja kati ya yale ambayo anaamini yangeangaziwa zaidi anapotafuta kuongeza ushawishi wake barani Afrika.

Wadadisi wa tasnia ya burudani nchini Uganda wanahisi kwamba migogoro kati ya wasanii na waandalizi wa matamasha inazidi kuongezeka na mara nyingi huishia kwa kutupiliwa mbali kwa matamasha.

Hata baada ya changamoto hiyo, Spice anasema bado amejitolea kuhakikisha anarejea Uganda kukutana na mashabiki wake.

Share This Article