Speed Darlington aishtaki NAPTIP mahakamani

Hii ni baada ya shirika hilo kutangaza Darlington anasakwa kwa makosa ya ubakaji, unyanyasaji wa mtandaoni na kuvizia watu mitandaoni.

Marion Bosire
1 Min Read
Speed Darlington

Mwanamuziki wa Nigeria Darlington Okoye maarufu kama Speed Darlington ameshtaki shirika la kitaifa la kuzuia ulanguzi wa watu nchini Nigeria NAPTIP.

Darlington kupitia kwa mawakili wake, amewasilisha kesi katika mahakama moja ya Abuja akidai fidia ya Naira bilioni 3 kwa kuharibiwa sifa na shirika hilo lililomtangaza kama mtu anayesakwa.

Katika kesi hiyo, msanii huyo anasema kwamba hatua iliyochukuliwa na NAPTIP ilimharibia sifa na kumweka hatarini mitandaoni na nje ya mitandao.

Anataka mahakama izuie shirika hilo la kupambana na ulanguzi wa binadamu, kuchukua hatua kuhusiana na tangazo lake la Juni 27 la kumsaka.

Haya yote yanatokana na video iliyosambaa mitandaoni inayomwonyesha Darlington akikiri kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtoto.

Shirika la kushughulikia dhuluma za nyumbani na za kijinsia katika jimbo la Lagos lilichukua hatua za haraka kushughulikia video hiyo kabla ya kuwasilisha kesi hiyo kwa NAPTIP, iliyomtangaza kuwa mtu anayesakwa.

Katika tangazo hilo kwenye Instagram, NAPTIP ilielezea kwamba Darlington alikuwa akisakwa kwa makosa ya ubakaji, unyanyasaji wa mtandaoni na kuvizia watu mitandaoni.

Darlington tayari amekanusha madai hayo akisema kwamba video hiyo haikustahili kuchukuliwa kwa uzito kwani yeye ni msanii na wasanii huhitaji utata ili kustawi.

Msanii huyo pia aliomba msamaha kwa yeyote ambaye alikwazika na video hiyo.

Share This Article