Rais William Ruto, ameelezea kujitolea kwake kuongoza taifa hili na kufanikisha maendeleo kupitia mabadiliko, akisema hana sababu ya kukosa kutimiza majukumu yake.
Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi alipokutana na viongozi kutoka kaunti ya Tharaka Nithi, Rais alisema tajiriba yake, elimu na maisha ya awali ya mashinani yanampa fursa nzuri ya kushughulikia changamoto zinazokumba taifa hili.
“Wengine walionitangulia labda walikuwa na sababu za kutochukua hatua, wengine labda wangelaumu elimu yao, wengine umri au maswala yanayowakumba wakenya,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa taifa alitaja muda wa miaka 15 akiwa mbunge na mwongo mmoja akiwa Naibu wa Rais, kama nyadhifa zilizomtayarisha kwa wadhifa wa Urais.
“Sijakula chumvi nyingi, nina elimu ya kutosha, na nimetoka mashinani. Ninaelewa matatizo ya nchi hii kikamilifu,” aliongeza Rais.
Aidha, alieezea mipango ya serikali yake kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo, kuimarisha uchumi wa nchi, kufanyia mageuzi sekta ya afya na kuboresha miundomsingi.
“Hili ndilo jukumu ambalo lazima nitekeleza,” alisema kiongozi wa taifa, huku akitoa wito kwa wakenya kuendelea kumuombea anapoliongoza taifa hili.