Simba wa Teranga wanyonyoa vipungu wa Nigeria, michuano ya CHAN

Senegal wanaongoza kundi hilo kwa pointi 3, wakifuatwa na Congo na Sudan kwa alama moja, kisha Nigeria wanashika nanga pasi na alama.

Dismas Otuke
1 Min Read

Mabingwa watetezi wa kombe la CHAN, Simba wa Teranga kutoka Senegal, walianza vyema utetezi wa kombe lao kwa ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Nigeria.

Mchuano huo wa kundi D ulisakatwa jana usiku uwanjani Amaan, kisiwani Zanzibar.

Pande zote zilibuni nafasi haba katika mchuano huo huku kipindi cha kwanza kikimalizikia sare tasa.

Derby hiyo ya Afrika Magharibi ikielekea sare tasa, Super Eagles wa Nigeria walifanya makosa katika safu ya nyuma na kumpa Christian Gomis, fursa ya kufyatua tobwe la chini pembeni kushoto na kupachika bao pekee na la ushindi kunako dakika ya 75.

Ushindi huo uliwaweka Teranga Lions, kwenye nafasi bora ya kufuzu kwa robo fainali, wakihitaji ushindi mmoja katika mechi mbili zilizosalia dhidi ya Congo na Sudan kuafikia ndoto hiyo.

Upande wao Super Eagles ni sharti waishinde Sudan, katika mechi ya pili Agosti 12, ili kufufua matumaini ya kuingia hatua ya mwondoano.

Nigeria wanarejea kwenye kipute hicho kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2018.

Senegal wanaongoza kundi hilo kwa pointi 3, wakifuatwa na Congo na Sudan, kwa alama moja, kisha Nigeria wanashika nanga pasi na alama.

 

Share This Article