Fainali ya Makala ya nane ya kipute cha kombe la CHAN Jumamosi hii itakuwa kati ya Simba wa milima ya Atlas kutoka Morocco, dhidi ya Ngómbe wa Zebu wa Madagascar, katika uwanja wa Kasarani.
Morocco waliotwaa kombe hilo mwaka 2018 na 2020, walijikatia tiketi kwa fainali baada ya kuwacharaza Senegal penalti 5-3, kufuatia sare ya bao moja katika nusu fainali iliyosakatwa uwanjani Mandela jijini Kampala,Uganda jana usiku.
Layousse Samb aliwaweka mabingwa watetezi Simba Teranga, kifua mbele kunako dakika ya 16, kabla ya Sabir Bougrine, kusawazishia Simba wa Atlas kutoka Morocco dakika saba baadaye.
Timu zote zilitoka sare baada ya dakika 120 na kubidi matuta yachongwe ili kuwatenganisha Simba hao wawili.
Mohamed Hrimat, Oussama Lamlioui, Ayoub Khairi, Anas Bach na Youssef Mehri, waliunganisha penalti za Morocco.
Vieux Cisse, Baye Ciss na Daouda Ba walifunga penalti za Senegal huku Seyni Mbaye Ndiaye, akipoteza mkwaju wake.
Awali, katika nusu fainali ya kwanza, Madagascar waliomaliza mechi wakiwa wanandinga 10 uwanjani waliwabwaga Sudan bao moja kwa bila katika muda wa ziada kufuatia sare tasa katika dakika 90 uwanjani Benjamin Mkapa nchini Tanzania.
Toky Rakotondraibe alifunga bao hilo dakika ya 116, huku Madagascar, wakifuzu kwa fainali kwa mara ya kwanza.
Madagascar watacheza fainai ya kombe hilo kwa mara ya kwanza huku Morocco wakiwania kombe la tatu.