Silver Concert ya Jaydee kuandaliwa Ijumaa hii

Msanii huyo wa Tanzania anaadhimisha miaka 25 katika tasnia ya muziki.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Judith Wambura maafuru kama Lady Jaydee ataandaa tamasha lake la Silver Ijumaa hii Juni 13, 2025.

Amekuwa akitoa tangazo hilo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii anapoadhimisha miaka 25 katika tasnia ya muziki almaarufu Silver Jubilee.

Jaydee aliingilia tasnia ya muziki mwaka 2000 wakati huo akiwa na umri wa miaka 20 pekee na miaka miwili tu baadaye, akaibuka kuwa mwanamuziki bora wa kike wa mtindo wa R&B nchini Tanzania.

Alishinda tuzo ya albamu bora ya R&B kwenye tuzo za muziki za Tanzania mwaka 2004.

Mzaliwa huyo wa eneo la Shinyanga ni mmoja kati ya wanamuziki ambao wamesalia wima katika tasnia ya muziki huku wengi alioanza nao wakilegea.

Wasanii wanaotarajiwa kutumbuiza kwenye tamasha lake Ijumaa katika ukumbi wa Superdome ulioko Masaki jijini Dar es Salaam ni pamoja na Rapcha, Papii Kocha, Patricia Hillary, Joh Makini na Domokaya.

Wengine ni AY, Fid Q, Frida Amani, Wakazi na Malkia Karen na tamasha hilo litaandaliwa katika maeneo mengine katika siku zijazo kama vile Dodoma na Mwanza tarehe 20 na 27 mwezi huu mtawalia.

Zoezi jingine ambalo msanii huyu amekuwa akiendeleza kama sehemu ya sherehe za miaka 25 katika tasnia ni maandalizi ya nyimbo mpya.

Ameandika pia kitabu kuhusu maisha yake ambacho amekipa jina la “Diary ya Lady Jaydee – Kurasa za Majaribu na Ushindi” ambacho kitazinduliwa rasmi kesho Alhamisi Juni 12, 2025.

Share This Article