Mbunge wa Kinangop Kwenya Thuku ametetea msimamo wake wa kisiasa akisema kuwa hana cha kujuta kwa kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza.
Kwenya amesema kuwa ingawaje alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Jubile, ataendelea kuunga mkono utawala wa Rais William Ruto ili aweze kufanikisha miradi ya maendeleo katika eneo bunge lake.
Akzungumza wakati wa hafla ya kuzindua rasmi miradi iliyofadhiliwa na hazina ya NGCDF Kinangop, mbunge huyo amesema kuwa kwa sasa wananchi hawana haja na siasa zisizo na manufaa, ila tu wanataka kuona miradi ya maendeleo, na ndiposa alikata kauli ya kuunga mkono serikali ili kufanikisha hayo.
Amewataka wananchi kukoma kuwafuata viongozi ambao wanajihusisha katika siasa potovu, huku akiwataka kuwapiga msasa viongozi waliochaguliwa kwa misingi ya miradi ya maendeleo ambayo wanatekeleza mashinani.
Wananchi katika maeneo ya Munyaka – Gathaara na Ragia-Nyakio alikozindua miradi ya maabara na ukumbi wa mikutano wamesema kwamba miradi hiyo itachangia pakubwa kuinuia kiwango cha elimu katika eneo bunge la Kinangop.
Zaidi ya hayo, wameunga mkono kauli ya Kwenya kuhusu siasa wakisema kwamba wanachohitaji kwa sasa ni miradi ya maendeleo.
Kulingana na wananchi hao, ifikapo uchaguzi wa mwaka 2027, watafanya uamuzi wao wenyewe bila kushinikizwa na mawimbi ya kisiasa kwa kuegemea vyama au kabila.