Gavana wa kaunti ya Nyeri Mutahi Kahiga ameendelea kukosolewa kutokana na matamshi yake yaliyoonekana kudhihaki kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.
Wa hivi karibuni kuwaonya wanaomkosea Raila heshima ni Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki.
“Aliyekuwa Waziri Mkuu ameenda kupumzika akiwa na amani na akiwa ameridhiana na watu wote wa taifa letu la Kenya na wapinzani wote ambao alikuwa nao, wapinzani wa kisiasa. Kwa hivyo kusiwe na mtu wa kwenda kuleta matusi, kudharau au kumkosea heshima mwenzetu ambaye ameenda mbele za haki na ambaye Mungu amemuita akapumzike,” alisema Prof. Kindiki wakati akiwahutubia wakazi wa kaunti ya Pokot Magharibi.
“Hilo ni jambo la kuleta fedheha na aibu kwa kiongozi yeyote kuleta matamshi ya kudharau, kukejeli, ama kusherehekea eti kifo cha mwenzetu ambaye ni kiongozi ametumikia taifa letu kwa miaka mingi.”
Shutuma dhidi ya Gavana Kahiga pia zimetolewa na Tume ya Taifa ya Uwiano na Maridhiano, NCIC.
Tume hiyo kupitia mwenyekiti wake Dkt. Samuel Kobia imemshutumu Gavana Kahiga kutokana na matamshi yake ikiyataja kuwa yasiyostahili hasa wakati huu ambapo Wakenya wanaomboleza kifo cha Raila ambaye atakumbukwa daima kama shujaa wa taifa.
“Maneno haya situ kwamba yalikuwa ya kizembe, yasiyojali hisia za wengine, na yenye madhara makubwa, lakini pia yanakuja wakati ambapo Wakenya wanaomboleza kifo cha kiongozi shupavu,” alisema Dkt. Kobia kwenye taarifa.
“Mheshimiwa Raila Odinga alikuwa siyo tu shujaa wa taifa lakini pia kiongozi wa bara la Afrika na dunia ambaye maadili yake ya kisiasa na huduma zake kwa taifa bila kujinyima ziliongoza mustakabali wa kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa kipindi cha miongo minne.”
Dkt. Kobia akiongeza kuwa matamshi kama hayo siyo tu kwamba yanamkosea heshima kiongozi ambaye alikuwa shujaa wa taifa lakini pia yanaweza yakachochea uhasama wa kikabila.
Akiwahutubia wanahabari kufuatia shutuma zinazoongezeka dhidi yake, Gavana Kahiga ameomba msamaha akisema matamshi yake hayakudhamiria kuikosea familia ya marehemu wala Wakenya heshima.
Aidha, Kahiga ametangaza kujiuzulu kama Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, wadhifa ambao alivuliwa na baraza hilo wakati wa mkutano wake usiokuwa wa kawaida mapema leo Jumatano asubuhi.
Viongozi mbalimbali wamemkemea Gavana Kahiga huku wengine wakidai yeye ni nembo ya upinzani ambao umekuwa ukieneza semi za chuki.
Chama cha ODM kilichoongozwa na marehemu Raila Odinga pia kimelaani vikali matamshi ya Gachagua kikiyataja kuwa ya kikatili.
“Chama cha ODM kinaelezea masikitiko yake makubwa na ghadhabu kutokana na matamshi ya kizembe, yenye kuleta migawanyiko na kufedhehesha yaliyotolewa na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga wakati wa tukio moja la umma huko Kieni – matamshi ambayo yalionekana kudhalilisha na hata kusherehekea kifo cha kiongozi wetu Raila Amolo Odinga, C.G.H,” alisema Nassir kwenye taarifa.
“Wakati ambapo mamilioni ya Wakenya bila kujali mirengo ya kisiasa, kikabila na kidini bado wanaomboleza, Gavana Kahiga aliamua kuongeza chumvi kwenye makovu ya wazi ya taifa.”
Kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah pia amemkosoa Gavana Kahiga kwa kutoa matamshi hayo ya kizembe.
“Kahiga, tutakuombea. Matamshi ya kizembe na kikatili kiasi gani? Nakosa maneno ya kukuambia lakini ikizingatiwa nilipatwa na msiba hivi karibuni, nafahamu kile ambacho naweza nikafanya sasa ni kukuombea mno,” alisema Ichung’wah ambaye pia ni mbunge wa eneo bunge la Kikuyu, kaunti ya Kiambu.
“Kukuombea kwamba Mwenyezi Mungu akupe hekima kiasi na kuomba kwamba hukuzungumza kwa niaba ya mkubwa wako kwa sababu waropokaji huonekana kurudia kile walichokisikia mkubwa wao akisema.”
Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru pia amezishutumu kauli za Kahiga akizitaja kuwa zisizofaa.
“Kauli zilizotolewa na mwenzangu, Gavana wa Nyeri siyo kwamba hazifai, zinakosa kuzingatia hisia za wengine na zinakosa uwajibikaji,” alisema Waiguru ambaye ameshutumiwa na upande wa upinzani kutoka eneo la Mlima Kenya katika siku za hivi karibuni.
“Kauli hizo haziakisi maoni ya uongozi au watu wa Mlima Kenya,” aliongeza Waiguru akisema eneo la Mlima Kenya linaungana na nchi nzima katika kumwomboleza Raila.
Mwingine aliyeshutumu matamshi ya Kahiga ni mwenyekiti wa chama tawala cha UDA Cecily Mbarire.
“Wakati ambapo taifa letu linaomboleza, taarifa kama hizo siyo tu za kizembe lakini zinazokosa heshima, siyo tu kwa kumbukumbu ya Mkenya shupavu bali pia kwa mamilioni ya Wakenya wanaoomboleza,” alisema Mbarire ambaye pia ni Gavana wa Embu.
“Wacha ieleweke vizuri: Kauli za Gavana Kahiga haziakisi maoni ya eneo la Mlima Kenya.”