Shughuli ya kuutazama mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Raila Odinga imekamilika katika uwanja wa Mamboleo kaunti ya Kisumu.
Mamia ya wakazi walijitokeza katika uwanja huo kuutazama mwili huo, wakimpa kiongozi huyo heshima za mwisho kabla ya mazishi yake siku ya Jumapili.
Jeneza la Raila ambalo lilikuwa limepambwa na bendera ya taifa, lilibebwa na helikopta ya jeshi kuelekea nyumbani Bondo.
Awali mwili wa Raila ulikuwa usafirishwe kwa barabara lakini kamati ya kitaifa ya maandalizi ya mazishi ya Raila, ikabadili mpango huo na kuamua kuwa usafirishwe kwa ndege.
Katibu wa wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo alithibitisha kuwa mwili wa Raila utasafirishwa kwa ndege kutoka Mamboleo hadi Bondo kutokana na sababu za kiusalama.
Aidha, Omollo alisema hatua hiyo iliafikiwa baada ya mashauriano ya kina kati ya Kamati andalizi ya kitaifa na familia ya marehemu Raila Odinga.
Mwili wa Raila utakesha nyumbani kwake Bondo, huku familia na marafiki wa karibu wakiruhusiwa kuutazama nyumbani kwake.
Ibada ya mazishi ya Raila itaandaliwa katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga.