Shughuli ya kupiga kura yaanza katika maeneo mbali mbali

Marion Bosire
2 Min Read

Shughuli ya kupiga kura imeanza katika maeneo 24 kunakoandaliwa chaguzi ndogo leo Novemba 27, 2025.

Kulingana na tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC wakazi wa kaunti ya Baringo wanachagua Seneta wao leo. Wadhifa huo ulisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Seneta William Cheptumo.

Wakazi wa maeneo bunge ya Banissa, Kasipul, Magarini, Malava, Mbeere North na Ugunja nao wanachagua wabunge wao leo. nyadhifa hizo zilisalia wazi kufuatia kufutiliwa mbali kwa matokeo ya uchaguzi au vifo vya waliokuwa wakizishikilia.

Wadi 17 pia zinachagua wawakilishi wao katika mabunge ya magatuzi husika na ni pamoja na wadi ya Angata Nanyokie kaunti ya Samburu, wadi ya Chemundu/Kapng’etuny kaunti ya Nandi na wadi ya Chewani kaunti ya Tana River.

Nyingine ni wadi ya Fafi kaunti ya Garissa, Kariobangi North kaunti ya Nairobi, Kisa East katika kaunti ya Kakamega, Metkei katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, Mumbuni North kaunti ya Machakos na Narok Town katika kaunti ya Narok.

Orodha hiyo inakamilishwa na wadi ya Purko katika kaunti ya Kajiado, Tembelio kaunti ya Uasin Gishu, Nyansiongo, Nyamaiya na Ekerenyo za kaunti ya Nyamira, Kabuchai/Chwele katika kaunti ya Bungoma, Lake Zone na Nanaam katika kaunti ya Turkana.

Nyingi kati ya chaguzi hizo zilichelewa kwa muda mrefu kufuatia utokuwepo kwa tume kamili ya uchaguzi kwani wengi wa makamishana wa IEBC walijiuzulu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Share This Article